Mfanisi anaanza safari yake ya kujisaka punde akiwa shuleni katika madarasa ya malezi na chekechea. Anatembea katika dunia hii ambayo anajiona akiwa pekee katika ulimwengu wa familia za wazazi wote wawili, kinyume naye aliye na mama pekee. Dunia yake inampelekea kuwa na marafiki tofautitofauti kuanzia Moi's Bridge huko Kenya, Mwanza Tanzania na mara tena Nakuru na Mombasa nchini Kenya. Maisha yake, kimsingi yanaathiriwa pakubwa na ama marafiki zake au familia yake. Katika riwaya hii utakumbana na maudhui mseto yanayoathiri kizazi cha leo na kijacho. Imeyaangazia maudhui mbalimbali kama vile maisha katika ndoa, mahusiano ya vijana kwa vijana, mahusiano ya wazee kwa vijana na wazee kwa wazee, talanta, elimu, bidii na kazi, usaliti katika maisha, unafiki, siasa na uongozi n.k. Ni kazi inayomulika maisha ya leo na jinsi masuala ibuka yanavyoathiri jamii kwa namna hasi au chanya na ni kazi ya aina yake na ambayo hutajutia kuiweka mkononi kuisoma.