Tungo nyingi zilizomo humu ziliandikwa baina ya robo ya mwisho ya mwaka 2010 na nusu ya mwanzo ya mwaka 2015. Hii ni miaka mitano ya mwanzo ya mshairi kuhamia na kuishi nchini Ujerumani - mbali na nyumbani kwao, Zanzibar. Ndani yake, kwa hivyo, muna muakisiko wa hisia za mgeni ugenini, akitayamani mengi mazuri ya kwao na akijutia kuyaacha nyuma yake. Ukweli ni kuwa wakati mtu anapoishi ugenini, ndipo hasa ile thamani ya kwao anapoitambua na kutaka kuitambulisha navo zaidi na zaidi. Ndipo hisia za kutambuwa kuwa ana kwao zinapopanda kiwango cha juu. Kutoka kipembe cha mbali, Mohammed Ghassanani anakuangalia kwao na kuyaona mambo ambayo alipokuwamo ndani yake, alikuwa hata hajui kama yapo. Chembilecho Wajapani: "Samaki hajijui kuwa amerowa!" Na sababu ya kutokujijuwa huko, kwa hakika, ni kwa kuwa yeye mwenyewe anaishi ndani ya maji muda wote.
Mohammed Ghassani alizaliwa kisiwani Pemba mwaka 1977, ambako alikulia na kusomea had alipohamia kisiwani Unguja kwa ajili ya masomo na maisha mwaka 1996 a mwaka 2010 akahamia nchini Ujerumani, ambako ndiko anakoishi na kufanya kazi