Mji wa Kambare ni diwani iliyotungwa kwa umahiri na ustadi wa aina yake kuweza kumvutia kila anayeisoma, awe ni mwanafasihi na mwanaisimu ama mtu wa fani yoyote ile. Hii inatokana na uteuzi mzuri wa misamiati inayolandana vina na mizani kiasi ya kuukonga moyo wa msomaji. Muwala, ufundi mkubwa katika kupangilia maneno, ujenzi wa taswira na lugha ya picha, ubobezi katika kumfikirisha msomaji, upana wa dhamira na maudhui yapatikanayo katika tungo zilizomo ndani ya diwani hii zinagusia takriban nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Kwa kiasi kikubwa, diwani hii imetumia lahaja za kizanzibari, hasahasa kipemba. Pia kuna maneno ya Kiswahili asilia ambayo yametumika kuongeza vionjo vya lugha na utamu wa michapo ya mashairi na tungo za Kiswahili cha uswahilini. Hata hivyo, maneno magumu yamefafanuliwa maana mwishoni ili kukidhi haja ya msomaji wa diwani hii. Kwa ujumla, diwani hii itawafaa sana wapenzi wa lugha ya Kiswahili hususani wapenzi wa mashairi, walumbi wa lugha, wanataaluma, wanafunzi wa ngazi tofauti za elimu, walimu shuleni, wakufunzi vyuoni, wafanyakazi maofisini na taasisi mbalimbali za kielimu, asasi za kijamii, vikundi vya tamaduni na sanaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vikundi vya ngoma za burudani. Hapana shaka, maendeleo ya lugha na Ushairi wa Kiswahili pamoja na ukuaji wake unaonekana waziwazi endapo utajisomea diwani hii.